Chama cha kihafidhina cha Ujerumani cha Christian Democratic Union, CDU kimeshinda uchaguzi katika jimbo la Schleswig-Holstein. Takwimu rasmi za matokeo ya awali yaliyotolewa mapema leo zimekiweka chama hicho katika nafasi ya kwanza na asilimia 43.4 ya kura, hatua kubwa mbele kuliko asilimia 32 ya kura ilizopata katika uchaguzi wa mwaka 2017. Chama cha Kijani kimeshika nafasi ya pili kikishinda asilimia 18.3 ya kura huku chama kinachopendelea wafanyabiashara cha FDP kikishika nafasi ya nne na asilimia 6.4 ya kura. Chama cha Social Democratic SPD kikiongozwa na mgombea wake Thomas Losse-Müller kimepata asilimia 16 ya kura. Waziri Mkuu mashuhuri Daniel Günther wa chama cha CDU sasa ana fursa kadhaa za kuunda serikali ya mseto. Anaweza kuendelea na serikali ya sasa ya mseto na chama cha Kijani na FDP, lakini mseto wa vyama viwili unawezekana pia.