Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanachama wake
kuhakikisha wanalinda dola kwa kufanya kazi na kutekeleza Ilani na ahadi
zote wakati wa uchaguzi.
Kimesema kuwa wananchi ambao ndio wapiga
kura zinazomuweka madarakani rais, wabunge na madiwani ndio waajiri na
wanaostahili kutumikiwa kikamilifu na hapo ndipo Chama kitaendelea
kulinda dola na sio kwa silaha.
Akizungumza kwenye mkutano wa ndani
wa wanachama wa CCM mkoani Kilimanjaro, Shaka amesema kamwe huwezi
kulinda dola kwa kutumia silaha.
“Hamuwezi kulinda dola kwa marungu
na mapanga, zaidi tunapaswa kutekeleza kwa vitendo yale yote tuliyoahidi
wakati wa uchaguzi. Tunapofanya vizuri hapo tunakuwa na uhakika wa
kuendelea kushika dola,” amesema Shaka.
Shaka ambaye ameongozana na
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana
kwenye ziara ya kukagua uhai wa chama mkoani hapa, amewaambia wanachama
wa chama hicho kuwa hakuna sababu ya kutofanya vizuri kwenye uchaguzi
mkuu 2025.
“Hakuna sababu ya kukosea 2025 kwa sababu ya Rais
tuliyenaye (Samia Suluhu Hassan) Mungu ametupa kwa ajili ya kutatua
shida za wananchi. Mungu ametupa Kinana ambaye anakijua vyema chama na
anamsaidia mwenyekiti (Rais Samia) kutattua shida za Watanzania,”
amesema Shaka ambaye ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kupuuza
uzushi kuhusu usafiri wa treni kati ya Dar es Salaam na Kilimanjaro.
“Kumekuwa
na propaganda kuwa tangu ameingia Rais Samia huduma za treni
zimesimama...huo ni uongo wa mchana kabisa. Nataka kuwaambia kuwa
Serikali itafanya matengenezo makubwa ya njia ya treni na Chama
tumeelekeza ikamilishe haraka matengenezo hayo.” amesema.
Amesema
wananchi wa Kilimanjaro wawe tayari kusafirisha mazao yao nje ya nchi
baada ya Rais Samia kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi na baadhi
yatatumia treni.