Mbunge wa Kilindi (CCM), Omary Kigua ameitaka Serikali kutoa vibali vya ajira kwa wateule wa Rais wanaowaondoa watumishi waliowakuta katika taasisi wanazopangiwa kuongoza.
Kigua ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 22, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mwaka 2022/2023.
Kigua amesema kuna baadhi ya watu wanaoteuliwa na Rais huwaondoa watumishi hadi 30 kwenye taasisi na kuomba vibali vya kuleta watumishi wengine.
Alimuomba katibu mkuu wa ofisi hiyo kutokubali kutoa kibali cha kuajiriwa watumishi wengine kwa sababu wengine ni waandamizi katika nafasi zao na kwamba halina afya.
Hata hivyo, mbunge wa Nachingwea (CCM), Dk Amandus Chinguile alimpa taarifa kuwa wapo watumishi ambao wanakaimu kwa zaidi ya miaka miwili.
Amesema wanapokuja viongozi wengine huwaondoa na kuwaacha katika magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo sonona na presha.
Akiendelea kuchangia Kigua amesema kuwa dhana hiyo sio nzuri na haina afya kwa taasisi husika ambapo ameshauri wajenge utamaduni wa kuwaamini watumishi wao.
Amesema katika jimbo lake la Kilindi wapo watumishi ambao wana elimu ya darasa la saba ambao wamefanya kazi kwa miaka zaidi ya 20.
Amesema kati yao wapo waliostaafu lakini hawajapata pensheni zao kwasababu ya kukosa sifa.
“Watanzania hawa uliwaambia wafanye kazi za utendaji wa vijijini, na hivi ninavyoongea mkurugenzi wa halmashauri ameshaleta barua ofisini kwako miezi sita sasa haina majibu. Naomba jambo hili lifanyiwe kazi,”amesema.