Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainabu Katimba amehoji juu ya waajiri wasiotoa fursa kwa watumishi wao kufanya kazi wakiwa karibu na wenza wao.
Katimba amehoji suala hilo leo Alhamisi Aprili 14, 2022 Bunge jijini Dodoma, “Nini kauli ya Serikali juu ya waajiri ambao hawatoi fursa ya kuhakikisha watumishi wao wanapata haki ya kufanya kazi wakiwa karibu na wenza wao”
Akijibu swali hilo Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema Katibu Mkuu wa ofisi yake ametoa waraka wenye masharti ya kumuhakikishia mtumishi anapata kibali cha kumfuata mwenza wake.
Hata hivyo, amesema hilo litafanyika endapo eneo husika litakuwa na nafasi na uwepo wa uthibitisho wa ndoa na nyaraka nyingine.
“Nitoe wito kwa waajiri wote kuzingatia kifungu cha waraka huo, ili kusaidia ustawi wa familia, malezi ya watoto na kuhakikisha kuwa wafanyakazi wetu wanakuwa na nafasi ya kuishi na wenza kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa,”alisema.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Husna Sekiboko alihoji athari kwa watumishi wenza kuishi mbali na watoto.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanahamis Ali Khamis amesema kuna madhara ya kijamii katika jamii kwa watumishi wenza kuishi mbali na watoto wao.
Ameyataja madhara hayo ni kuongezeka kwa vitendo vya ukatili kwa watoto majumbani, kukosa malezi chanya yanayopelekea watoto kuathirika kisaikolojia.