Urusi yataka kikao cha Baraza la Usalama kuhusu uhalifu wa mjini Bucha

Urusi imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya kikao leo Jumatatu, kujadili ilichokiita ''uchokozi wa Waukraine wenye msimamo mkali'' katika mji wa Bucha, baada ya serikali ya Ukraine kuwatuhumu wanajeshi wa Urusi kuuwa raia katika mji huo. Moscow imekanusha kuhusika na mauaji ya raia, ikisema huenda picha za maiti mitaani zinazoenezwa katika vyombo vya habari ni za uongo. Ukraine imesema kuwa imegundua miili ya raia 410 katika maeneo iliyoyachukua kutoka kwa wanajeshi wa Urusi katika mkoa wa Kiev. Meya wa mji wa Bucha Anatoly Fedoruk ameliarifu shirika la habari la AFP kuwa walilipata kaburi la halaiki ilimozikwa miili ya watu 280. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ameshtushwa na picha zinazotoka katika mji wa Bucha, na ametaka uchunguzi huru ufanyike na waliohusika kuwajibishwa.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii