Viongozi wanaohasimiana Sudan Kusini wamesaini makubaliano kuhusu kifungu muhimu cha kijeshi cha mpango wa amani unaosuasua. Makubaliano hayo yamefikiwa jana kutokana na upatanishi wa nchi jirani ya Sudan. Pande hizo mbili zimekubaliana kuanzisha kamandi ya pamoja ya jeshi, suala muhimu ambalo kwa muda mrefu limekwamisha utekelezaji wa mkataba wa mwaka 2018 wa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vilivyodumu kwa miaka mitano. Martin Abucha aliyesaini makubaliano hayo kwa niaba ya chama cha upinzani cha SPLM/A-IO amesema amani inatokana na usalama na wamepiga hatua muhimu. Waziri katika ofisi ya rais wa Sudan Kusini, Barnaba Marial Benjamin amepongeza makubaliano hayo, kama hatua muhimu inayofungua njia ya kuwa na serikali imara ya Jamhuri ya Sudan.