Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan aitisha uchaguzi mpya

Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ameitisha uchaguzi mpya baada ya bunge kutupilia mbali kura ya kutokuwa na imani naye. Rais wa Pakistan Dr. Arif Alvi ameukubali ushauri wa Waziri mkuu Imran Khan na amelivunja bunge. Kwa mujibu wa ofisi ya rais uchaguzi huo sasa utafanyika katika muda wa siku 90. Khan alipoteza wingi wa viti bungeni baada ya washirika wake na wabunge kadhaa wa chama chake kuhamia upande wa upinzani. Endapo kura hiyo ingefanyika, kungehitajika kura 172 katika bunge lenye viti 342 ili kumwondoa madarakani, nyota huyo wa zamani wa mchezo wa Kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa. Hata hivyo spika wa bunge Qasim Suri alitupilia mbali hoja hiyo akisema vyama vya upinzani vilikuwa na njama ya kumwondoa madarakani waziri mkuu vikisaidiwa na mataifa ya nje. Imran Khan anailaumu Marekani kwa kuwaunga mkono wapinzani wanaotaka kumwangusha.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii