Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameombea ulimwengu kuonyesha wema na huruma zaidi kwa wakimbizi wakati alipokutana na wahamiaji nchini Malta. Francis ameyasema hayo katika siku ya pili na ya mwisho ya ziara yake nchini Malta kwa kutembelea pango la Mtakatifu Paulo huko Rabat. Inaaminika kuwa mitume wa Yesu walikaa kwenye pango hilo baada ya meli yao kuharibika wakiwa njiani kuelekea Roma. Francis ametumia ziara hiyo kusisitiza tena wito wake kwa Ulaya kuonyesha ukarimu sawa kwa wahamiaji na wakimbizi hasa wanaokimbia vita nchini Ukraine. Kwa muda mrefu Malta imekuwa katikati ya mjadala juu ya sera yake ya wakimbizi. Nchi hiyo yenye watu nusu milioni mara kwa mara imekosolewa na mashirika ya misaada ya kibinadamu kwa kukataa kuruhusu meli za uokoaji kutia nanga kwenye bandari zake.