ICC yafungua ofisi Venezuela kuchunguza ukiukaji wa haki za binaadamu

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai - ICC imefungua ofisi nchini Venezuela kama sehemu ya uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binaadamu wakati wa maandamano ya kuipinga serikali katika mwaka wa 2017. ICC ilianzisha uchunguzi rasmi kuhusu madai hayo ya ukiukaji wa haki Novemba mwaka jana na kusaini mkataba wa maelewano na Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ambao ulisema kuwa nchi hiyo ya America Kusini itachukua hatua za kuhakikisha mahakama hiyo itaweza kufanya kazi yake. Akizungumza pamoja na Maduro katika ikulu ya Rais mjini Caracas, Mwendesha mashitaka wa ICC Karim Khan amesema ni hatua muhimu na kubwa itakayomuwezesha kutekeleza majukumu yake. Zaidi ya watu 100 waliuawa mwaka wa 2017 wakati vikosi vya usalama viliyakabili maandamano yaliyochochewa na ukamataji wa viongozi kadhaa wa upinzani na uamuzi wa mahakama ya juu kabisa wa kulivunja bunge lililokuwa limethibitiwa na upande wa upinzani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii