Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan ameituhumu Marekani kwa kuingilia siasa za nchi yake -- madai ambayo yamekanushwa haraka na Washington. Khan alilihutubia taifa jana usiku, akisema nchi ya kigeni ambayo ni Marekani inataka Khan aondolewe madarakani. Mjini Washington, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Ned Price aliwaambia waandishi habari kuwa hakuna ukweli wowote katika madai hayo. Amesema Marekani inaheshimu na kuunga mkono mchakato wa kikatiba wa Pakistan na utawala wa kisheria. Hayo ni wakati mjadala wa kutokuwa na imani naye bungeni ukiahirishwa jana. Hakuna waziri mkuu wa Pakistan aliyewahi kukamilisha muhula wake madarakani, na Khan anakabiliwa na changamoto kubwa kabisa kwa utawala wake tangu alipochaguliwa mwaka wa 2018, huku wapinzani wakimtuhumu kwa usimamizi mbaya wa uchumi na kuvuruga sera ya kigeni.