Bunge la DRC lapiga kura ya kumtimua waziri wa uchumi.

Bunge la Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumatano limepiga kura ya kumuondoa kwenye wadhifa wake waziri wa uchumi Jean Marie Kalumba, likimshtumu kwa mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu na uratibu mbovu wa sekta ya uvuvi, kati ya masuala mengine.

Waziri huyo amepewa saa 48 ili awe amekwisha wasilisha barua ya kujiuzulu kufuatia kura hiyo ya kumuondolea imani.

Kalumba aliteuliwa kwenye wadhifa huo na Rais Felix Tshisekedi mwaka jana.

Hoja iliyotiwa saini na wabunge imeweka wazi malalamiko mengi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa sera ya kusaidia wavuvi na uhaba wa petroli wa mara kwa mara unaosababisha ongezeko la bei ya usafiri.

Kalumba hakupatikana mara moja kwa ajili ya maelezo.

Congo ni mzalishaji mkubwa wa shaba barani Afrika na mchimbaji mkubwa wa madini ya betri ya cobalt duniani, lakini inasalia kuwa mojawapo ya nchi maskini zaidi zenye maendeleo duni duniani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii