Mashabiki wa mchezo wa mpira wa miguu duniani wamenunua tiketi 804,186 za mechi za Kombe la Dunia nchini Qatar baadae mwaka huu katika awamu ya kwanza ya uuzajii
Shirikisho la Mpira wa Miguu FIFA na waandaaji wa michuano hiyo wamesema wanunuzi wengi wa tiketi hizo wametokea Qatar, Marekani, England, Mexico, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ujerumani, India, Brazil, Argentina na Saudi Arabia.
Tiketi za mechi ya ufunguzi mnamo Novemba 21 ambayo itaihusisha wenyeji Qatar pamoja na za fainali itakayofanyika Disemba 18, 2022 ndizo zilizonunuliwa kwa wingi.
Timu 32 zitashiriki michuano hiyo, mpaka sasa ni pekee 27 ndizo ambazo tayari zimefuzu. Droo ya mwisho ya Kombe la Dunia ambapo timu zitapangwa katika makundi itafanyika kesho siku ya Ijumaa ya Aprili mosi.