DK SAMUEL MUTASA KUZIKWA KAGERA

Mwili wa kikongwe aliyefanikiwa kupata shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 82, Dk Samuel Mutasa unatarajiwa kuwasili nchini Jumatano ya wiki ijayo kabla ya kusafirishwa kwenda kupumzishwa katika nyumba ya milele Bukoba mkoani Kagera.

Dk Mutasa alijipatia umaarufu mwaka 2020, wakati wa mahafali ya 50 ya chuo hicho alipofanikiwa kuhitimu Shahada ya uzamivu baada ya kuisotea kwa muda mrefu.

 Mtoto wa marehemu, Kemilembe Mutasa alisema wanatarajia mwili utawasili Jumatano ya wiki ijayo na kuagwa Alhamisi kabla ya kusafirishwa kwenda Bukoba vijijini mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi.

Akielezea namna kifo cha baba yake kilivyotokea, alisema Jumatano iliyopita baba yake akiwa nchini Marekani alikokwenda kusalimia watoto wake wengine alipata maradhi ya shinikizo la damu (presha kupanda) na kusababisha kupasuka kwa mshipa mmoja kichwani.

Alisema baada ya kuona hali yake imebadilika alimtumia mtoto wake ujumbe mfupi wa maneno akimtaka arudi nyumbani.

“Alipofika nyumbani alimkuta ameanguka akiwa amepoteza fahamu.

“Walijaribu kumuwahisha hospitali na madaktari waliendelea na matibabu, lakini hali iliendelea kuwa mbaya na kufariki Jumatatu Machi 28,” alisema Kemilembe.

Alisema kwa sasa taratibu za mazishi na msiba kwa ujumla zipo nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam.

Dk Mutasa alitunukiwa PhD katika uchambuzi wa kemikali katika mimea lishe na dawa, safari ambayo aliianza miaka 41 kabla ya kutunukiwa shahada hiyo mwaka 2020 na Mkuu wa UDSM, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii