Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Rais Uhuru Kenyatta amekaribisha rasmi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye umoja huo.
Uhuru Kenyatta Aongoza EAC Kuikaribisha Rasmi Jamhuri ya Congo katika Jumuiya ya Kikanda
Akizungumza wakati wa Mkutano wa 19 Extra-Ordinary Summit uliofanyika Jumanne, Machi 29, Uhuru alipongeza uamuzi uliotolewa na nchi wanachama wa jumuiya ya kuikubali DR Congo.
"Katika zaidi ya miaka 50 iliyopita, tuliazimia kufikia ulimwengu wa utandawazi kama kambi. Leo tunajadili ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kujiunga na jumuiya yetu. Ningependa kuzipongeza nchi wanachama na viongozi wote kwa kuafikia hatua hii ya uamuzi,” alisema Rais Uhuru.
DRC lilipewa nafasi katika jumuiga hiyo baada ya kupigwa msasa mkali na maafisa wa mataifa yenye uanachama katika EAC.
Uhuru alisema nchi iliomba kujiunga na jumuiya hiyo Februari 2018 na kupata uanachama huo baada ya kukidhi vigezo vyote hitajika.
Huu ni wakati wa kihistoria katika jumuiya na Afrika kwa ujumla. Inadhihirisha uwezo wa EAC kujitanua nje ya mipaka yake na kutumia masoko yaliyopo kwa ukuaji wa uchumi," alisema.
Umoja huo sasa unajivunia kuwa na nchi wanachama saba zikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na DR Congo.
Nchi inakuja pamoja na rasilimali zake ambazo zinaweza kutumiwa na jamii katika kupanua masoko yake.
Bwawa la umeme la Inga lingesambaza kanda na zaidi ya MW 60,000 safi inayohitimisha mjadala wa ni wapi pa kujenga mabwawa ya kuzalisha umeme katika eneo hilo.
"Kwa watu wanaotafuta ustawi, hili ni suala muhimu sana. Tunakaribisha DRC katika EAC,” alisema Uhuru.
Rais wa Kenya alibainisha kuwa jumuiya itafanya kazi katika kurejesha amani nchini, akiongeza kuwa "sehemu ya eneo hilo imekuwa na matatizo kwa muda."
Mkutano huo ulihudhuriwa na marais Samia Suluhu (Tanzania), Yoweri Museveni (Uganda) Paul Kagame (Rwanda), Evariste Ndayishimiye (Burundi), Salva Kiir (Sudan Kusini) na Felix Tshisekedi wa DR Congo.