Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken jana ameizuru Morocco ambako alizungumzia Sahara Magharibi, maendeleo na usalama wa kikanda. Ziara hiyo imefanyika baada ya Blinken kuhudhuria mkutano wa kilele wa kikanda na Israel ambako alikutana na viongozi wa Israel na mataifa ya Kiarabu. Akizungumza na waandishi habari mjini Rabat, Blinken amesema Marekani inatambua janga linalosababishwa na upungufu wa usambazaji wa bidhaa. Blinken alikuwa akimaanisha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambao umesababisha kupanda kwa bei ya ngano na mafuta, hilo likiwa pigo kubwa kwa nchi za Afrika Kaskazini zinazotegemea uagizaji wa bidhaa. Akiwa Morocco, Blinken alikutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Aziz Akhannouch, Waziri wa Mambo ya Nje, Nasser Bourita pamoja na mrithi wa kiti cha ufalme wa Abu Dhabi, Mohammed bin Zayed al-Nahyan. Leo Blinken anatarajiwa kuizuru Algeria.