Macron ajitenga na matamshi ya Biden kuhusu Putin

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameonya dhidi ya kuongezeka kwa mvutano wa maneno na Urusi, baada ya Rais wa Marekani, Joe Biden kumuelezea Rais wa Urusi, Vladmir Putin kama "mchinjaji". Macron amekiambia kituo cha utangazaji cha France 3, kwamba hatotumia maneno hayo. Kiongozi huyo wa Ufaransa amesisitiza kuwa kila kitu kinapaswa kufanyika ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi, ikiwa kuna matumaini ya kusitisha vita vya Urusi nchini Ukraine. Macron amesema jukumu lake ni kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kisha majeshi ya Urusi kuondoka kabisa kwa kutumia njia za kidiplomasia. Usiku wa Jumamosi, akiwa ziarani mjini Warsaw, Poland, Biden alimuita Putin "mchinjaji" na hapaswi kuendelea kubakia madarakani. Hata hivyo baadae, Ikulu ya Marekani ilisema nchi hiyo haitaki mabadiliko ya utawala Urusi. Adha, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema mabadiliko ya utawala nchini Urusi, sio lengo la Jumuia ya Kujihami ya NATO, licha ya uvamizi wake nchini Ukraine.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii