Will Smith Amzaba Kofi Mc Tuzo Za Oscar

MWIGIZAJI maarufu wa Holywood, Will Smith (53), usiku wa jana alifanya tukio lisilo la kawaida, baada ya kumzaba MC wa Tuzo za Oscar, Chris Rock katika tuzo hizo zilizokuwa zinafanyika katika Ukumbi wa Dolby Theatre, Hollywood nchini Marekani baada ya Rock kumtania mkewe, Jada Pinkett.

Licha ya tukio hilo, Smith alitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo za Oscars katika kipengele cha mwigizaji bora wa mwaka, kupitia filamu ya King Richard ambayo ameigiza kama baba wa nyota wa mchezo wa tenisi duniani, Venus na Serena Williams.

Katika kipengele hicho, Smith alikuwa akipambana na mastaa wengine wakali akiwemo Denzel Washington ambapo katika ‘speech’ yake baada ya kutangazwa mshindi, alimwaga machozi na kuomba radhi kwa kitendo alichokifanya.

Sababu kubwa ya Smith kumzaba MC Rock, ni baada ya mchekeshaji huyo kumtania Jada kuhusu mtindo wake wa nywele wa upara ambao haukumpendeza Smith na mkewe.

Rock alisikika akisema anampenda Jada huku akisema anaisubiri sehemu ya 2 ya filamu ya G.I. Jane. Kwa ambao hawajaelewa. G.I. Jane ni filamu ya mwaka 1997 iliyomuonesha mwigizaji Demi Moore akiwa na upara.

Mwanzo wa utani huo, Smith alichukulia poa na kutabasamu, lakini Rock alipoendelea, hakupendezwa na hata Jada alionekana kupandwa na hasira kwa sababu miaka ya karibuni, mwanamama huyo amekuwa akipambana na tatizo la kupoteza nywele (Alopecia).

Tatizo hilo limesababisha awe ananyoa nywele zote kichwani na baada ya kuikubali hali hiyo, amekuwa kama balozi wa watu wenye tatizo hilo duniani kote hivyo kitendo cha Rock kumtania, kiliwakasirisha wote wawili, Jada na mumewe na kumfanya achukue uamuzi uliowashangaza wengi wa kwenda kumpiga kibao Rock akiwa jukwaani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii