Chama cha Social Democratic, SPD kimetangazwa mshindi katika uchaguzi wa jimbo la magharibi mwa Ujerumani, Saarland. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na vituo vya utangazaji vya ARD na ZDF, chama hicho cha Kansela Olaf Scholz kimeshinda uchaguzi wa jimbo hilo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20, kwa kupata asilimia 43.5 ya kura. Bodi ya uchaguzi ya serikali imesema chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU kimepata asilimia 28.5 ya kura. Tangu mwaka 1999 jimbo la Saarland limekuwa likiongozwa na CDU chama cha kansela wa zamani, Angela Merkel. Katika uchaguzi huo wa jana, SPD ilipata viti 29 kati ya 51, hivyo kuwa na wingi wa kura. Anke Rehlinger wa SPD, sasa atakuwa waziri mkuu mpya wa jimbo la Saarland, akichukua nafasi ya Tobias Hans wa CDU.