Raia wa Zimbabwe wamepiga kura jana Jumamosi katika uchaguzi muhimu wa bunge na manispaa, unaoonekana kuwa ni kipimo kwa chama tawala cha Rais Emmerson Mnangangwa kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwakani. Kumekuwa na hamasa kubwa kuelekea uchaguzi huo ambapo rais Mnangagwa aliongoza mikutano mbalimbali ya kampeni kuvutia uungwaji mkono kwa wagombea wa chama chake cha ZANU-PF. Hata hivyo kulionekana misusuru mifupi muda mfupi baada ya kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura mapema jana asubuhi. Chama kipya kilichoundwa na kiongozi wa upinzani Nelson Chamisa kimeonekana kuvutia makundi mbalimbali ya watu nchini humo. Wakosoaji na upande wa upinzani wanamtuhumu rais Mnangagwa kwa kuwaandama wapinzani wake na wana mashaka iwapo uchaguzi huo utakuwa wa haki.