Kabul, Watawala wa Taliban nchini Afghanistan katika hatua ya kushangaza na isiyotarajiwa, wameamua kutozifungua tena shule za wasichana na kwenda kinyume na ahadi walioitoa ya kuruhusu wasichana kusoma. Uamuzi huo uliothibitishwa na afisa wa Taliban, unarudisha nyuma juhudi za Taliban kutambuliwa kimataifa na hata kupokea ufadhili katikati ya mzozo mkubwa wa kiuchumi unaoukumba nchi hiyo ya Asia. Jamii ya kimataifa imewahimiza viongozi wa Taliban kufungua shule na kuruhusu wasichana na wanawake kupata haki ya elimu. Mashirika ya misaada yamesema hatua hiyo imezidisha hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wa Afghanistan katika wakati uongozi wa Taliban unaonekana kuyumba kutokana na mizozo ya ndani kwa ndani. Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa Deborah Lyons anatarajiwa kukutana na uongozi wa Taliban leo Alhamisi kuwataka kubadilisha uamuzi wao.