Wanaharakati Jamaica wadai fidia za ukoloni wa Uingereza

Mwanamfalme wa Uingereza William na mkewe Kate wamewasili Jamaica kama sehemu ya ziara yao eneo la Carribean, saa chache baada ya wanaharakati kuandamana wakidai fidia kutokana na dhulma enzi za ukoloni. Ziara ya mwanamfalme huyo inaambatana na miaka 70 ya uongozi wa Malkia Elizabeth, ziara hiyo itakamilika kwa William na mkewe kuizuru Bahamas. Mamia ya watu walikusanyika nje ya ubalozi wa Uingereza mjini Kingston, na kubeba mabango yaliyoitaka Uingereza kuomba msamaha kutoakana na madhara yaliyotokea wakati wa ukoloni. Mwanaharakati aliyeandaa maandamano hayo Dokta Rosalea Hamilton, amesema kuna makosa ya kihistoria yaliyofanyika na yanapaswa kushughulikiwa. Ziara ya Mwanamfalme huyo inaonekana kama juhudi za kushawishi koloni za zamani za Uingereza ikiwemo Belize na Bahamas kuwa sehemu ya utawala wa ufalme wa Uingereza katikati ya ongezeko la vuguvugu la kutaka mataifa hayo kuwa huru kabisa badala ya kuwa chini ya jumuiya ya madola ambapo Malkia Elizabeth ndio mkuu wa dola hizo. Jamaica inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru mnamo mwezi Agosti.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii