RATIBA KAMILI YA MECHI ZITAKAZO CHEZA ROBO FAINALI YA UEFA

Mabingwa watetezi Chelsea watamenyana na mabingwa mara 13 Real Madrid katika robo fainali ya Kombe la Klabu Bingwa barani Ulaya.
Mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza Manchester City watachuana na mabingwa wa Uhispania Atletico Madrid ambao waliwabandua majirani Manchester United katika hatua ya 16 bora wiki hii ugani Old Trafford.
Liverpool watamenyana na Benfica ya Ureno huku Bayern Munich wakiwa na kibarua dhidi ya Villarreal ya aliyekuwa kocha wa Arsenal Unai Emery.
Katika hatua ya nusu fainali, mshindi kati ya Chelsea na Real Madrid atamenyana na bingwa kati ya Atletico Madrid na Manchester City huku atakayeibuka bora kati ya Benfica na Liverpool akichuana na mshindi kati ya Villarreal na Bayern Munich.
Mkondo wa kwanza wa mechi za robo fainali umeratibiwa kuchezwa Aprili 5-6 huku mkondo wa pili ukiwa Aprili 12-13.
Katia hatua ya nusu fainali, mkondo wa kwanza utachezwa kati ya Aprili 26-27 huku mkondo wa upili ukiratibiwa kuchezwa Mei 3-4.
Uwanja wa Stade de France jijini Paris utaandaa fainali ya mashindano hahyo mnamo Mei 28 baada ya kuhamishwa kutoka St Petersburg kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Droo hii inamaanisha kuwa Chelsea watakutana na aliyekuwa kocha wao Carlo Ancelotti ambaye aliwaongoza kushinda taji la EPL na kombe la FA kwa msimu mmoja alipohudumu kama kocha wao kati ya mwaka 2009 na 2011.
Chelsea na Real Madrid zilikutana katika nusu fainali msimu jana, kocha Thomas Tuchel akiwaongoza vijana wake kuibwaga Real 3-1 kwa ujumla kabla ya kuinyuka Manchester City 1-0 katika fainali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii