Poland inasema zaidi ya wakimbizi milioni mbili, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamewasili nchini humo tangu kuanza kwa mapigano nchini Ukraine. Maafisa wa ulinzi wa mpakani wa Poland wanasema hapo jana tu kulikuwa na zaidi wakimbizi 52,000 kutoka Ukraine, idadi hiyo ikiwa imepungua kwa asilimia 11 ikilinganishwa na juzi. Walinzi hao vile vile wanasema zaidi ya watu laki mbili wamevuka mpaka huo na kuingia Ukraine tangu Februari 24, wengi wao wakiwa wamejitolea kupigana na majeshi ya Urusi. Hakuna taarifa rasmi kuhusiana na idadi ya wakimbizi waliosalia Poland na waliosafiri kuelekea katika nchi zengine za Umoja wa Ulaya.