Kampuni ya Microsoft imesema wataalamu wake wanaendelea na juhudi za kiufundi kurejesha huduma zake kwa wateja wake baada ya mamilioni ya watumiaji wa huduma za kampuni hiyo kuripoti changamoto.
Watumiaji wa Microsoft katika nchi za Marekani, Japan, Singapore, Uingereza na Australia ndio waliokuwa wa kwanza kuripoti kushindwa kupata huduma za kampuni hiyo kabla ya watumiaji katika mataifa mengine kuripoti kuathiriwa.
Watumiaji wameripoti kupata shida ya kutumia huduma za kampuni hiyo kama Teams, Outlook na huduma nyengine muhimu.
Zaidi ya watu milioni 430 duniani wanatumia huduma za Microsoft 365, ambazo ni huduma za usajili zinazojumuisha Outlook na Teams.
Uongozi wa kampuni ya Microsoft wakati ukiripoti wataalamu wake kuendelea na juhudi za kurejesha huduma za kawaida, haujahusisha changamoto hiyo na shambulio la kimtandao.