Zaidi ya abiria 40 wamenusurika kifo baada ya basi la Kampuni ya Abood, lenye namba za usajili T.285 EAV, kuteketea kwa moto wakati likisafiri kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Kagera.
Tukio hilo limetokea leo Novemba 13, 2026 majira ya saa 11 alfajiri katika eneo la Isaka, Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama, SSP Stanley Luhwago, amesema jeshi hilo lilipokea taarifa za tukio hilo na kufika eneo la tukio, ambapo lilifanikiwa kuuzima moto huo.
Amesema hakuna abiria aliyejeruhiwa katika tukio hilo, huku jeshi hilo likifanikiwa kuokoa mali na mizigo ya abiria waliokuwa ndani ya basi hilo.
Aidha, ametoa wito kwa wamiliki wa mabasi na madereva kuhakikisha vyombo vyao vya usafiri vinakuwa na vifaa vya kuzimia moto vinavyofanya kazi vizuri ili kukabiliana na majanga ya moto yanayoweza kujitokeza wakati wa safari.
Hata hivyo, chanzo cha moto huo pamoja na thamani ya hasara iliyosababishwa na tukio hilo bado havijafahamika.
Tukio hilo linaendelea kukumbusha umuhimu wa kuzingatia taratibu za usalama wa vyombo vya usafiri ili kulinda maisha ya abiria na mali zao.