Umoja wa mataifa umekadiria kuwa zaidi ya watu 323,000 wamekimbia mapigano kati ya jeshi la Congo na wapiganaji waasi wa kundi la FRN huko Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, katika siku nne zilizopita, wakati huu Shughuli kadhaa za misaada zikiwa zimesimamishwa, Jeshi likidai kusimamisha kusonga mbele kwa FRN.
Katika ripoti iliyochapishwa na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya kibinadamu Novemba 11 ni kuwa mapigano yanayoendelea mkoani Kivu kusini mashariki mwa DRC kati ya vikosi vya jeshi la serikali FARDC vinavyoshirikiana na wazalendo, na wapiganaji wa harakati ya kisiasa-na kijeshi inayoongozwa na rais wa zamani Joseph Kabila na kuungwa mkono na Kigali, yamesababisha zaidi ya watu laki tatu na ishirini na watatu 323,000 kutoroka makazi yao, kati ya Novemba 6 na 9 maeneo mawili ya Kivu Kusini, Kalehe na Kabare, kaskazini magharibi mwa Bukavu.
Wengi wakikabiliwa na ukosefu wa misaada ya kibinadamu, mahema, na chakula, huku baadhi yao wakikimbilia maeneo yenye usalama mdogo, huko walipokelewa na jamaa zao, wengine walitafuta hifadhi katika shule, sehemu za ibada, au vituo vya afya, na Wengine walikimbilia msituni au karibu na Hifadhi ya Taifa ya Kahuzi-Biega, katikati ya msimu huu wa mvua.
Huku hayo yakijiri huko Bunyakiri, jeshi la Kongo FARDC limesema limezuia kusonga mbele kwa washambuliaji Hao wa FRN.
Ofisi ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa iliripoti Jumatano asubuhi kwamba mapigano yalikuwa yakiendelea kuzunguka kijiji cha Chaminunu, katika eneo la Kalonge, na yalikuwa yakikaribia eneo la Shabunda, wakati huu Umoja wa Mataifa umesema kuwa umesikitishwa kuona mapigano tayari yanazuia harakati za timu kadhaa za kibinadamu kuwafikia watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu.