MAMILIONI ya wafanyakazi nchini Hispania wameingia katika mgomo wa kitaifa Jumatano, Novemba 11, 2026, wakishinikiza Serikali kuchukua hatua kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha na mgogoro wa upatikanaji wa nyumba.
Mgomo huo, ambao ni wa kwanza wa kitaifa nchini humo ndani ya miaka 14, umeathiri sekta mbalimbali zikiwemo usafiri wa umma, viwanda na biashara, huku ukifanyika zikiwa zimesalia chini ya wiki tatu kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 29.
Mvutano ulianza katika soko la jumla la Mercamadrid jijini Madrid, ambako waandamanaji wapatao 1,000 walikusanyika kupinga hali ngumu ya maisha. Chama cha wafanyakazi cha CCOO kilidai kuwa polisi walitumia gesi ya pilipili kuwatawanya waandamanaji na kumkamata mtu mmoja, huku watu 13 wakihitaji matibabu.
Katika jiji la Barcelona, baadhi ya barabara zilifungwa na matairi kuchomwa moto. Vyama vya wafanyakazi vya UGT na CCOO viliripoti kuwa ushiriki wa mgomo katika sekta za magari na bandari ulifikia asilimia 90.
Moja ya sababu kuu za mgomo huo ni kupanda kwa gharama za makazi, ambapo kodi za nyumba zimekaribia kuongezeka mara mbili ndani ya kipindi cha miaka 10.
Benki Kuu ya Hispania inakadiria kuwa nchi hiyo ina upungufu wa nyumba takribani 750,000, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuvuka milioni moja ifikapo mwaka 2028.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, kodi ya wastani ya nyumba nchini humo ni euro 1,176 kwa mwezi, kiasi kinacholingana na asilimia 98.7 ya mshahara wa wastani wa kila mwezi wa kijana.