Rais Samia Suluhu Hassan atashiriki na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Geita katika hafla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli itakayofanyika Machi 17, 2022 katika Uwanja wa Magufuli uliopo mjini Chato.
Baadhi ya viongozi watakaoshiriki hafla hiyo ni makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi pamoja na viongozi mbalimbali wa nchi.
Hayo yameelezwa leo Jumapili Machi 13, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyemule wakati akiwasalimia waumini wa Kanisa la KKKT Usharika wa Upendo mjini hapa na kuwataka wajitokeze kushiriki hafla hiyo.
Senyamule amesema Serikali kwa kushirikiana na familia ya hayati Magufuli wamekusudia kufanya kumbukumbu ya mwaka mmoja ikiwa ni njia ya kumkumbuka kiongozi huyo.
Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka 2021 katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es salaam baada ya kuugua maradhi ya moyo.