Kundi la wananchi katika eneo la Fela wilayani Misungwi mkoani Mwanza unapojengwa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), kati ya Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga, limesimamisha msafara wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu huku wakitoa kilio cha kunyimwa ajira katika mradi huo.
Wananchi hao ambao wamekita kambi katika eneo hilo tangu mwaka 2021 wamezuia msafara huo leo Jumatatu Machi 14, 2022 saa 10:40 asubuhi na kusababisha wajumbe wa kamati hiyo kusimama na kuwasikiliza kilio chao.
Mwenyekiti wa wananchi hao, Paulo Mnema amesema pamoja na wananchi hao kutoka maeneo tofauti nchini kukaa muda mrefu bila kupewa ajira katika mradi huo, pia amedai kuna urasimu katika ajira zinazotolewa kwani baadhi yao wanaombwa rushwa ili kupatiwa ajira hizo.
"Mheshimiwa hapa kuna shida, tuko hapa tangu mwaka jana bila kupatiwa ajira kuna watu wanaletwa kutoka kwenye miradi mingine wanafika wanahonga fedha wanapewa ajira sisi tupo tunasubiria, tunateseka kwa sababu tunakula kwa tabu kwani hatuna hela na ajira, tunaomba mtusaidie," amesema Mnema.
Akizungumza baada ya kusikiliza kilio cha wananchi hao, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Seleman Kakoso ameahidi kufikisha kilio chao serikalini.
Awali Mwenyekiti huyo alikutana na kilio kingine cha wananchi wa eneo la Fela wanaodai kutolipwa fidia ya maeneo yao zaidi ya Sh800 milioni licha ya kufanyiwa tathmini ya mashamba yao yaliyochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Veronica Kessy amekiri wananchi hao kutolipwa fidia huku akisema kinachokwamisha ni taratibu za malipo.
"Ni kweli wananchi hawajalipwa fidia kinachokwamisha ni taratibu za kimalipo, ila zianfanyiwa kazi kufiki Mei 14 mwaka huu watakuwa wameanza kulipwa fidia yao," emesema Kessy
Reli hiyo yenye urefu wa kilometa 341 inaanzia Fela wilayani Misungwi mkoani Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga huku ikitarajia kugharimu zaidi ya Sh3 trilioni.