Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umemshauri Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza Oktoba 29 ya kila mwaka kuwa Siku ya Kitaifa ya Kumbukizi ya Wahanga wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mtandao huo umesema siku hiyo itatoa fursa kwa taifa kuwakumbuka watu waliopoteza maisha, kuwafariji familia zilizoathirika na kutafakari hatua za kuzuia matukio kama hayo yasijirudie.
Katika taarifa iliyotolewa jana, Mratibu wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema kumbukizi hiyo haipaswi kuwa ya maombolezo pekee, bali pia iwe sehemu ya juhudi za kutafuta ukweli, kuimarisha haki na uwajibikaji, kuponya majeraha ya walioathirika na kujenga mshikamano wa kitaifa.
“Tunawakumbuka wahanga, tunajifunza kutokana na historia, na tunachukua hatua kuhakikisha yasijirudie tena,” amesema.
Pendekezo hilo linazingatia pia mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.
Kwa mujibu wa THRDC, tume hiyo ilipowasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ilipendekeza Serikali kutenga siku maalumu ya maombolezo ya kitaifa kwa ajili ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha katika matukio hayo.
THRDC imesisitiza kuwa kumbukizi hiyo inapaswa kuwahusisha familia za wahanga, taasisi za umma, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wananchi, huku shughuli zikifanyika katika ngazi za taifa, mikoa na wilaya.
Shughuli zinazopendekezwa ni pamoja na ibada na sala, dakika za ukimya, kusikiliza ushuhuda wa hiari wa familia zilizoathirika, pamoja na kongamano la kitaifa litakalojadili ukweli, haki, maridhiano na njia za kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu.