Rangi zenye madini ya risasi zahatarisha afya za watoto

Rangi za mafuta zenye madini ya risasi zinaweza kuathiri ubongo, figo na mfumo wa uzazi, huku watoto, wajawazito na mafundi wa upakaji rangi wakiwa katika hatari ya kuathiriwa na sumu hiyo.

Daktari wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Amana, Grace Mhando, amesema watu wanaweza kuathiriwa kwa kuvuta vumbi la rangi inayochubuka au kumeza chembechembe za risasi kupitia mikono iliyochafuliwa.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Kimataifa ya Kuzuia Sumu ya Risasi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, amesema tafiti zinahitajika kubaini kiwango ambacho sumu hiyo inachangia matatizo ya kiafya, ikiwemo changamoto za ukuaji wa watoto.

L

Katibu wa Asasi ya Agenda, Dorah Swai, amesema kiwango cha rangi zilizobainika kuwa na risasi nchini kimepungua kutoka asilimia 77 hadi asilimia 13 kutokana na juhudi za udhibiti na ushirikiano na Serikali, wazalishaji na mashirika ya kimataifa.

Amesema Agenda imekuwa ikipima rangi tangu mwaka 2009, akisisitiza kuwa kiwango cha risasi katika rangi za majumbani hakipaswi kuzidi sehemu 90 kwa milioni.

“Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu “Kutoka Kutambua Kwenda Kuzuia” yanasisitiza udhibiti wa rangi na bidhaa nyingine zenye risasi, ulinzi wa wafanyakazi na tafiti za madhara ya kemikali hiyo kwa afya za wananchi,” amesema Dorah.

Ofisa Programu wa Agenda, Silvani Mng’anya, amesema pamoja na mafanikio hayo, ufuatiliaji wa watu ambao huenda tayari wameathirika na udhibiti wa bidhaa nyingine zenye risasi vinapaswa kuimarishwa.

Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu cha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Yohana Nanai, amesema dalili za kuathiriwa na risasi zinaweza kufanana na magonjwa mengine, hivyo vipimo maalumu na historia ya kazi ya mtu ni muhimu kubaini chanzo.

Mkaguzi wa Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA), David Elisha, amesema wazalishaji wanapaswa kupunguza viambata hatari kwenye bidhaa, huku wakitoa taarifa za usalama kwa mujibu wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Meneja Uzingatiaji Sheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Hamadi Kissiwa, amesema baadhi ya mafundi wa upakaji rangi na wanaoshughulika na betri za magari hufanya kazi bila glavu na barakoa, hivyo elimu na ushirikiano wa wadau vinahitajika kuimarisha usalama.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii