Rais wa Marekani Joe Biden ameimarisha uhusiano na Colombia kwa kuiteuwa nchi hiyo ya Amerika Kusini kuwa mshirika mkuu wa Marekani asie mwanachama wa NATO, na hivyo kufungua milango kwa ushirikiano wa karibu wa kijeshi na kibiashara. Biden ametoa tangazo hilo wakati wa ziara ya rais wa Colombia Ivan Duque mjini Washington, ambapo ameilezea Colombia kama mshirika muhimu. Duque amesema uteuzi huo umeupeleka uhusiano kati ya mataifa hayo kwa ngazi ya juu kabisaa, na kuishukuru Marekani kwa ushirikiano wake hasa katika mapambano dhidi ya Covid-19, baada ya Biden kuahidi kuipatia nchi hiyo msaada wa ziada wa dozi milioni mbili za chanjo ya Covid. Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wao, Biden amesema mataifa hayo mawili yamekubaliana kusaidia kurejesha demokrasia nchini Venezuela. Hadhi ya Mshirika mkuu asie mwanachama wa NATO ni sifa ya kisheria ambayo Marekani imeitoa kwa mataifa 15, na inaruhusu upatikanaji wa faida fulani za kiulinzi na kibiashara, lakini tofauti na uanachama wa NATO, hahakikishi ulinzi wa kijeshi kutoka kwa Marekani.