IMF yasema vita vya Ukraine vitayaathiri mataifa ya Afrika

Mkuu wa shirika la fedha duniani IMF, Kristalina Georgieva, amekutana na mawaziri wa fedha wa mataifa ya Afrika jana Alhamisi, kujadili athari za uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine. Amesema mtazamo wa kiuchumi wa Afrika uko katika hatari ya kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta kutokana na vita hivyo. Mataifa ya Afrika pia yanaathiriwa na kupungua kwa mapato yatokanayo ya utalii na kupungua kwa upatikanaji wa huduma za kifedha. Georgieva amesema nchi nyingi zitalazimika kurekebisha sera zake, na kuongeza kuwa IMF iko tayari kuzisaidia nchi za Afrika kupunguza gharama za marekebisho yoyote ya kisera. Vita nchini Ukraine tayari vinapandisha bei ya ngano, na kusababisha hofu ya kutokea uhaba wa chakula. Urusi na Ukrane ni wauzaji wakubwa wa nafaka nje. Bei ya mafuta pia inapanda, na hivyo kusababisha mzigo kwa chumi dhaifu za mataifa ya Afrika.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii