Bujumbura yakubali kuwapokea watu waliofukuzwa nchini Marekani

Burundi imekubali kuwapokea watu waliofukuzwa nchini Marekani wakiwemo wafungwa na wahamiaji haramu, ikiwa ni nchi ya hivi punde ya Afrika kuingia kwenye mkataba na utawala wa rais Donald Trump kuhusu mpango huu utata.

Nancy Mutoni, msemaji wa rais Evariste Ndayishimiye, amethibitisha hatua hii ya Burundi, na kueleza kuwa nchi yake itakuwa tayari kupokea watu watakaofukuzwa kutoka Marekani, lakini wasiwe wameshtakiwa kwa makosa ya jinai na hawana ushirikiano na makundi ya kigaidi.

Licha ya kuingia kwenye mkataba huo na Marekani, serikali ya Burundi haijaweza wazi, idadi ya watu itakayowapokea, watakuja lini na kiwango cha fedha watakapochopokea kutoka kwa Marekani.

Hata hivyo, Mutoni ameeleza kuwa maandalizi yanaendelea ambapo serikali ya Burundi inapanga ni wapi watu hao watapewa makaazi, watakula nini na namna watakavyoishi na raia wa nchi yake.

Aidha, ameeleza kuwa watu hao watakuwa na haki ya kuomba uraia wa Burundi iwapo watakidhi vigezo na kuchangia kwa maendeleo ya nchi hiyo.

Burundi inajiunga na mataifa mengine ya Afrika zaidi ya 10 kama Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Ghana na mengine ambayo yameingia kwenye mpango huo wa kuwapokea na kuwapa makaazi watu waliofukuzwa Marekani.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii