Burkina Faso imezindua kiwanda chake cha kwanza cha kusafisha dhahabu ndani ya nchi hiyo, serikali ya kijeshi ikisema itasaidia nchi kupata thamani zaidi kutoka katika madini yake.
Kiwanda hicho, Raffinor BF, kipo katika eneo la Ouaga 2000 mjini Ouagadougou na kina uwezo wa kusafisha hadi tani 164 za dhahabu kwa mwaka.
Waziri wa Madini wa nchi hiyo, Yacouba Zabré, amesema Burkina Faso inaingia katika hatua mpya ya kusimamia rasilimali zake, na kwamba badala ya kuchimba dhahabu na kuiuza ikiwa ghafi pekee, nchi inataka kuisafisha, kuthibitisha ubora wake na kuongeza thamani yake ndani ya Burkina Faso.
Kwa mujibu wa waziri huyo, kusafisha dhahabu nchini humo kutatengeneza ajira zinazohitaji utaalamu na kurahisisha ufuatiliaji wa madini na fedha zinazotokana na maliasili hiyo.
Serikali pia inatarajia kiwanda hicho kusaidia kupambana na utoroshaji wa dhahabu, biashara haramu na utakatishaji fedha.
Kiwanda hicho kimejengwa katika eneo la hekta tano. Kina sehemu ya kuyeyusha dhahabu, maabara ya kupima ubora, maghala yenye ulinzi na kitengo cha kutengeneza vito. Kwa mujibu wa televisheni ya taifa ya RTB, mradi huo umegharimu faranga bilioni 11 za CFA, sawa na takribani Dola za Marekani milioni 19; ukiwa umefadhiliwa na serikali kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani.
Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, amesema nchi haiwezi kuendelea kutegemea uchimbaji na uuzaji wa malighafi pekee.
Dhahabu ni moja ya bidhaa kuu zinazouzwa nje ya nchi hiyo na chanzo muhimu cha mapato.