Zaidi ya watu 80, wengi wao wakiwa ni wanawake, wanaripotiwa kutoweka baada ya kutekwa nyara na makundi yenye silaha katika mashambulizi mawili tofauti yaliyotokea mwishoni mwa wiki Kaskazini mwa Nigeria.
Kwa mujibu wa taarifa za usalama, watu 47, wengi wao wakulima wanawake, walitekwa nyara Jumamosi katika jimbo la Niger walipokuwa wakivuna karanga. Siku iliyofuata, wanawake wengine 40 walitekwa nyara katika jimbo jirani la Zamfara.
Makundi hayo yenye silaha, yanayojulikana kama majambazi, yamekuwa yakihusishwa na matukio ya utekaji nyara kwa ajili ya kudai fidia pamoja na wizi wa mifugo. Mara kwa mara hushambulia vijiji, kuua wakazi na kuchoma nyumba baada ya kupora mali.
Ripoti kutoka nchini humo zinadai kwamba utekaji nyara umekuwa chanzo kikuu cha mapato kwa makundi ya uhalifu nchini Nigeria. Takwimu zinaonyesha kuwa mabilioni ya Naira yamelipwa kama fidia kwa watekaji katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Wakati huo huo, suala la usalama linatarajiwa kuwa mojawapo ya ajenda kuu katika uchaguzi ujao wa urais.
Licha ya serikali kudai mafanikio katika mapambano dhidi ya makundi yenye silaha, watafiti wanaonya kuwa ghasia na mashambulizi yanaendelea kuongezeka katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.