Papa Leo ataka dawa za kupunguza maumivu kwa wagonjwa

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, ameonya kwamba sheria yoyote ya kibinadamu haipaswi kuondoa uhai wa mtu akiwamo mgonjwa, badala yake, wahudumu wa afya watunze uhai wa mtu kwa imani na matumaini.

Papa Leo ametoa kauli hiyo katika Kituo cha Makaribisho cha Notre-Dame, nchini Ufaransa, ambako amefanya ziara ya kitume.

Katika hotuba yake, amewaambia wagonjwa kwamba wao sio mzigo na kamwe hawapaswi kuwa watumishi wa kifo kilichopangwa.

“Ninajua kwamba kwa baadhi yenu, kutokana na magonjwa fulani na wakati mwingine maumivu makali, upeo wa mtazamo unaweza kuonekana mweusi, usio na uhakika, bila njia ya kutokea.

“Lakini hakuna sheria ya kibinadamu inayopaswa kukufanya upoteze uhakika wa utu wako. Jaribio lolote la kuondoa uhai kwa kisingizio cha huruma ya uongo lazima likataliwe kabisa. Kuondoa uhai hakuwezi kuchukuliwa kuwa kawaida. Kile kilicho halali si lazima kiwe cha kimaadili,” Papa Leo ameonya.

“Kaka na dada wapendwa wagonjwa, ninataka kuwaambia, nyinyi si mzigo; nyinyi ni moyo unaodunda wa ubinadamu wetu na hazina ya thamani kwa Kanisa.

“Ninawasindikiza ninyi katika majaribu mnayopitia kwa maombi. Mawazo yangu yanawaendea wote ambao hawawezi kuwa hapa na ambao wanatufuatilia kutoka nyumbani kwao au vyumba vyao vya hospitali,” amesema.

Kwa upande wa wahudumu wa afya, amewataka wawe watumishi wenye shauku ya maisha na si kuyaondoa.

“Hapa Lourdes, jiji la wagonjwa na la matumaini, ninawaalika jumuiya nzima ya wafanyakazi wa afya kukumbuka maana kubwa ya wito wenu;  kumtunza mtu anayeteseka, na sio kuondoa uhai wake.

“Iweni watumishi wenye shauku ya maisha…dawa haiwezi kamwe kuwa mtumishi wa kifo kilichopangwa,” amesisitiza.

Ameongeza: “Ninawaalika, kuendeleza huduma za kupunguza maumivu na vituo vya utafiti; kwa upande mwingine, kuwasindikiza wagonjwa kwa upole, kama inavyotokea hapa Lourdes, ambapo madaktari, wauguzi, wabeba machela, mapadre, timu za wachungaji kwa wagonjwa na wengine wengi hutumia wito wao katika huduma ya utu wa mwanadamu, ili ulimwengu upate uzima.”

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii