Utalii unaendelea Mlima Kilimanjaro licha ya moto kuzuka

Moto mwingine umeibuka katika misitu ya Mlima Kilimanjaro, wiki tatu baada ya moto mwingine uliodumu kwa karibu wiki mbili kudhibitiwa, huku shughuli za utalii zikiendelea.

Katika taarifa yake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kitengo cha Mawasiliano, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Catherine Mbena, amesema moto huo umeanza alfajiri ya leo Jumatatu Septemba 28, 2029 katika eneo la Sangarini, karibu na mwinuko wa Kamwanga, kuelekea Shira Plateau, upande wa magharibi wa mlima Kilimanjaro.

Amesema timu ya pamoja inayojumuisha Zimamoto, maofisa uhifadhi, wadau wa utalii na wananchi, imepelekwa katika eneo hilo kudhibiti moto huo.

Katika taarifa hiyo, Mbena amesema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea kubaini kilichosababisha tukio hilo.

Vyombo vya habari vya kimataifa vimeripoti kuwa moto huo unaendelea katika eneo la Shira Plateau lililo katika urefu wa takribani mita 3,800 kutoka usawa wa bahari, huku juhudi za kuuzima zikikabiliwa na changamoto ya upepo mkali na uoto unaowaka kwa urahisi.

Hata hivyo, mamlaka zimesema shughuli za utalii, ikiwemo upandaji wa Mlima Kilimanjaro, zinaendelea kama kawaida.

Mbena amesema kuanza kwa msimu wa mvua katika baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Tanzania kunatoa matumaini kwamba moto huo utaweza kudhibitiwa haraka.

Tukio hilo limetoa muda mfupi baada ya moto mwingine katika upande wa mashariki wa mlima huo kuteketeza zaidi ya hekta 1,800 za uoto wa asili kabla ya kudhibitiwa.


Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii