Mashambulizi ya Urusi leo hii yanaelezwa kuyalenga maeneo ya raia huko katika mji wa katikati wa Ukraine Dnipro, huku vikosi vya wanajeshi hao wakiujongolea mji mkuu, Kyiv ambapo maafisa wamesema mji huo umegeuzwa kuwa ngome ya kijeshi.Mapema leo, ndege za kivita za Urusi zimefanya shambulizi lenye kuonekana kama la kwanza mjini Dnipro, na kuuwa mtu mmoja kwa mujibu wa kitengo cha huduma za dharura cha Ukraine.Kitengo hicho kimesema mashambulizi matatu ya anga yalilenga shule ya chekechea, jengo la makazi na kiwanda cha viatu. Kwengineko jeshi la Ukraine limeonya kuwa adui anajaribu kuondosha wanajeshi wake katika maeneo ya upande wa magharibi na kaskazini/magharibi mwa mji mkuu wa Kyiv.Hadi wakati huu maelfu ya raia wamekwama na mashambulizi yanaendelea kufanyika katika miji ya Ukraine, ikiwemo ya mji uliozingirwa wa Mariupol, baada ya mazungumzo kati ya wawaikilishi wa Moscow na Kyiv kumalizika hapo jana bila ya matunda yoyote.