Zambia yapiga kura, Hichilema akitarajiwa kuibuka mshindi

Raia wa Zambia leo wanapiga kura katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa, huku Rais Hakainde Hichilema akitarajiwa kushinda muhula wa pili wa uongozi.

Nchi hiyo ya kusini mwa Afrika yenye takriban wakaazi milioni 22 imefungua vituo vya kupigia kura saa 12:00 asubuhi, ambavyo vinatarajiwa kufungwa saa 12:00 jioni. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa Jumatatu.

Belinda Katanga, mkaazi wa Lusaka, ni miongoni mwa watu waliopiga kura leo.

"Nina furaha kupata fursa ya kutekeleza haki yangu ya kidemokrasia. Nina furaha sana."

Hichilema ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2021, anajivunia mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana katika muhula wake wa kwanza. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuiongoza Zambia katika mchakato wa marekebisho ya madeni kufuatia kushindwa kulipa deni lake la taifa mwaka 2020.

Zambia ni mmoja wa wazalishaji wakubwa wa shaba barani Afrika, na suala la uchumi limekuwa miongoni mwa ajenda kuu za kampeni za uchaguzi wa mwaka huu.

Mpinzani mkuu wa Hichilema ni Brian Mundubile, mbunge mkongwe ambaye anawania urais kwa mara ya kwanza. Mundubile anaongoza muungano wa vyama vya upinzani unaoungwa mkono na wafuasi wa rais wa zamani, marehemu Edgar Lungu.


 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii