UEFA Yaandaa Kesi ya Jinai Dhidi ya Infantino

Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) linajiandaa kuanzisha mchakato wa kisheria nchini Uswisi dhidi ya Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kwa tuhuma za usimamizi mbaya wa fedha, huku mashabiki wakimzomea na kumtukana wakati akiwakabidhi kombe washindi wa mashindano nchini Vietnam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nyaraka za kisheria zinaonyesha kuwa UEFA pamoja na wahusika wengine wanajiandaa kuwasilisha madai ya jinai dhidi ya Infantino na huenda viongozi au washauri wengine wa FIFA, wakihusisha suala hilo na tuhuma za “criminal mismanagement”.

Hatua hiyo inahusishwa na mpango uliokuwa ukihusisha FIFA kuuza hisa katika Kombe la Dunia, mpango ambao Infantino aliusitisha baada ya UEFA kutishia kususia mashindano hayo.

Wakati huo huo, Infantino alikumbana na hali ya aibu nchini Vietnam baada ya mashabiki waliokuwa kwenye Uwanja wa My Dinh National Stadium, Hanoi, kumtukana kwa lugha chafu alipokuwa akiwasilisha kombe baada ya Vietnam kuifunga Thailand na kutwaa ubingwa wa ASEAN.

Video kutoka uwanjani ilionyesha baadhi ya mashabiki wakimuita Infantino kwa matusi kwa lugha ya Kiingereza, huku rais huyo wa FIFA akitabasamu na kuwapungia mkono.

Infantino mwenye umri wa miaka 56 baadaye alielezea ziara hiyo kupitia Instagram, akisema matukio kama hayo yanaakisi kile ambacho FIFA inasimamia.

Infantino anatarajiwa kugombea tena nafasi ya urais wa FIFA katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 2027.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii