Infantino awania muhula mwingine, licha ya upinzani

Rais wa FIFA, Gianni Infantino, anaendelea kusukuma ajenda yake ya kugombea tena urais, akijipambanua kama mtetezi wa mataifa dhaifu kwenye kandanda.

Mkuu wa shirikisho la mpira barani Ulaya, UEFA, Aleksander Ceferin, amesema hatagombea dhidi yake, lakini anatarajia atakabiliwa na mpinzani katika uchaguzi wa Machi mwakani.

Ceferin alipinga vikali pendekezo la Infantino la kuuza sehemu ya haki za mashindano ya FIFA kwa wawekezaji binafsi, akisema linahatarisha mchezo kuliko hata mpango wa Super League.Mataifa madogo ya Ulaya pia yameungana kupinga mpango huo.

Infantino, ambaye anaungwa mkono na Afrika na Amerika Kusini, amesema FIFA inalenga kupunguza pengo kati ya mataifa tajiri na maskini kisoka, na kuleta fursa na uwekezaji kwa wanachama wote 211.

Ceferin anasema Ulaya si adui wa mataifa maskini, na amemkumbusha Infantino kuwa yeye pia ni Mzungu aliyeungwa mkono na UEFA hapo awali.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii