Serikali ya kijeshi ya Niger, inayoongozwa na Jenerali Abdourahamane Tiani kwa msaada wa washirika wake wa kijeshi kutoka Urusi, ilisema ilizuia uasi uliofanywa na baadhi ya wanajeshi
Kulingana na taarifa za vyombo vya habari na familia za waathiriwa, watu watano waliuawa katika machafuko hayo. Umoja wa Afrika pia umesisitiza wito wake wa kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba nchini Niger.
Katika taarifa yake, Mwenyekiti wa umoja huo Mahmoud Ali Youssouf, amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu mapigano yaliyotokea katika maeneo ya mji mkuu Niamey huku akisisitiza kuwa matumizi ya nguvu na vitendo vya kuvuruga utulivu wa taifa havipaswi kuvumiliwa, akitoa wito kwa pande zote kujizuia na kulinda usalama wa wananchi pamoja na uthabiti wa nchi.
Rais aliyepinduliwa Niger bado yupo kizuizini
Niger imekuwa chini ya utawala wa Jenerali Abdourahamane Tiani tangu mapinduzi ya Julai mwaka 2023 yaliyomuondoa madarakani rais aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Bazoum, ambaye bado anazuiliwa hadi sasa.
Bazoum, mwenye umri wa miaka 66, amekuwa chini ya ulinzi mkali katika makazi ya rais mjini Niamey tangu mapinduzi ya Julai 2023. Licha ya kukaa kizuizini kwa zaidi ya miaka miwili, Bazoum hajawahi kutangaza kujiuzulu na anaendelea kujitambulisha kama rais halali wa Niger.
Aliapishwa kuwa rais wa Niger Aprili 2, 2021 baada ya kushinda uchaguzi wa kidemokrasia kwa asilimia 55 ya kura.
Alikuwa rais wa kwanza nchini humo kuingia madarakani kupitia uhamisho wa mamlaka kwa njia ya kidemokrasia kutoka kwa rais mmoja aliyechaguliwa hadi mwingine. Hata hivyo, Julai 26, 2023, serikali yake iliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya jeshi yaliyoongozwa na Jenerali Abdourahamane Tiani.