Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, amezitaka mamlaka katika mikoa 14 kuchukua hatua za mapema za kujiandaa na kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotarajiwa kutokana na hali ya El Niño, ikiwa ni mara nyingine Tanzania inakabiliwa na hali hiyo baada ya El Niño ya msimu wa 2023/2024
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Septemba 2, 2026, Prof. Kabudi amesema maelekezo hayo yanatokana na utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) uliotolewa Agosti 18, 2026, unaoonesha uwezekano wa kutokea kwa El Niño yenye nguvu.
Amesema hali hiyo inaweza kusababisha mvua kubwa na madhara mbalimbali, ikiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, milipuko ya magonjwa, uharibifu wa miundombinu, makazi na mali.
Amebainisha Mikoa inyopaswa kuchukua hatua za maandalizi ni Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Mara, Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Aidha, amesema kuwa ingawa mikoa 14 imetajwa kuwa katika hatari zaidi ya kukumbwa na madhara ya El Niño, hatua za tahadhari na maandalizi zinapaswa kuchukuliwa na mikoa yote nchini ili kuhakikisha wananchi na miundombinu inalindwa dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.
Prof. Kabudi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu iliwaelekeza wakuu wa mikoa hiyo Agosti 26, 2026 kuanza maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza kutokea, huku akisisitiza umuhimu wa kutambua mapema maeneo hatarishi.
Aidha, amesema hatua hizo zinapaswa kuhusisha ukaguzi na uimarishaji wa miundombinu muhimu, ikiwemo madaraja, makaravati, mitaro, kingo za mito na mabwawa, pamoja na kuhakikisha vifaa vya uokoaji na huduma za dharura vinakuwa tayari.
Pia, amebainisha Kuwa serikali Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kukabiliana na Madhara ya El Niño unaohusisha hatua za kujiandaa, kuzuia na kupunguza madhara, kukabili maafa na kurejesha hali. Katika mpango huo, makadirio ya mahitaji kwa hatua zote nne yanafikia Shilingi bilioni 730, ikiwa ni pamoja na uokoaji, misaada na kurejesha miundombinu endapo madhara yatatokea.
Amefafanua kuwa Shilingi bilioni 730 si fedha zilizotengwa na Serikali, bali ni makadirio ya mahitaji ya mpango mzima. Amesema katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27, zimetengwa Shilingi bilioni 10 kwa ajili ya shughuli hizo kwa sekta zote, huku kiasi kitakachotumika kikitegemea ukubwa wa madhara yatakayotokea.
Pia, amewataka wananchi katika maeneo hayo kufuatilia taarifa rasmi za TMA, kuepuka shughuli katika maeneo hatarishi, kuweka akiba ya chakula na kuchukua hatua nyingine za kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.
Prof. Kabudi pia amevitaka vyombo vya habari kuendelea kutoa taarifa sahihi kuhusu utabiri huo ili kuelimisha wananchi, kuondoa taharuki na kuhakikisha jamii inachukua hatua kwa wakati.
Amesisitiza kuwa kukabiliana na El Niño si jukumu la Serikali kuu pekee, bali linahitaji ushirikiano wa serikali za mitaa, mikoa, sekta binafsi, mashirika, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla.