Polisi wachunguza kifo cha mwanafunzi aliyejirusha ghorofani

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Loreto, Stellah Wangaluke Shilingi (15), huku likitoa wito kwa wazazi, walezi na walimu kutambua mapema watoto wanaokabiliwa na changamoto za kisaikolojia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafugwa, amesema mwanafunzi huyo alifariki Agosti 31, 2026, baada ya kupata majeraha katika tukio lililotokea shuleni hapo, Mtaa wa Majengo Mapya, Kata ya Nyakato, Wilaya ya Ilemela.

Kwa mujibu wa Mtafugwa, mwanafunzi huyo akiwa na wenzake wakielekea kufanya usafi kabla ya kujirusha kutoka ghorofa ya kwanza.

Amesema mwanafunzi huyo alikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya matibabu, lakini ilibainika kuwa tayari alikuwa amefariki dunia.

Mtafugwa amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mwanafunzi huyo alikuwa akikabiliwa na msongo wa mawazo kwa muda mrefu kutokana na changamoto za kifamilia.

Aidha, amesema taarifa za awali zinaonyesha kuwa mwanafunzi huyo aliwahi kujaribu kujidhuru alipokuwa nyumbani wakati wa likizo ya mwezi Juni mwaka huu na kwamba shuleni alikuwa na tabia ya kujitenga.

Amefafanua kuwa kabla ya tukio hilo, mwanafunzi huyo aliacha ujumbe wa maandishi unaoeleza dhamira yake ya kutaka kujiua.

Wakati uchunguzi ukiendelea, Mtafugwa amesisitiza umuhimu wa wazazi, walezi na walimu kuwasikiliza watoto na kushughulikia changamoto zao mapema.

“Ni muhimu kuimarisha mifumo ya ushauri nasaha na malezi ya karibu, ili kuwatambua na kuwasaidia mapema vijana wanaokabiliwa na changamoto za kisaikolojia,” amesema.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limetoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wenzake na uongozi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Loreto kufuatia kifo hicho.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii