Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limebaini matukio ya wizi wa umeme katika maeneo ya Visiwani, Mwananyamala na Mivumoni, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wakati wa operesheni ya ukaguzi wa mita na miundombinu ya umeme.
Operesheni hiyo inalenga kudhibiti matumizi yasiyo halali ya umeme, kulinda miundombinu ya Shirika na kuhakikisha huduma ya umeme inatolewa kwa usalama na ufanisi.
Afisa Usalama wa TANESCO, Lilian Nizim, amesema wananchi wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu za matumizi ya umeme na kuepuka kuingilia au kuchezea mita.
“Mteja anapobaini changamoto yoyote inayohusiana na mita yake, anapaswa kutoa taarifa TANESCO ili ipatiwe ufumbuzi. Ni muhimu wananchi waepuke kabisa kuingilia mita kwa njia yoyote,” amesema.
Kwa upande wake, Mhandisi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Underson Manyika, amesema ukaguzi katika eneo la Visiwani ulibaini baadhi ya wateja wakichepusha nyaya za umeme, hali iliyosababisha mita kutosoma matumizi halisi.
“Ukaguzi wetu umebaini kuwepo kwa miunganisho isiyo halali iliyokuwa ikiathiri usomaji sahihi wa mita. Hatua stahiki zinaendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za Shirika,” amesema.
Manyika amesema wizi wa umeme husababisha hasara kwa Shirika, kuhatarisha usalama wa wananchi na kuathiri ubora wa huduma.
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na TANESCO kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi wa umeme na miunganisho isiyo halali ili hatua zichukuliwe kwa wakati.
TANESCO imeeleza kuwa itaendelea na ukaguzi wa mita na miundombinu ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika, salama na endelevu.