Iran yasema Marekani yatatiza kufikiwa makubaliano Vienna

Katibu wa Baraza Kuu la Kitaifa la Usalama la Iran, Ali Shamkhani, amesema Marekani haina nia ya kufikia makubaliano ya kuufufua mkataba wa nyuklia wa 2015 na Iran. Shamkhani amesema kwamba Marekani inasisitiza mapendekezo yasiyokubalika na kutaka makubaliano ya haraka kwa visingizio vya uwongo. Hata hivyo, afisa huyo hakufafanua zaidi mapendekezo ya Marekani. Afisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Masuala ya Kisiasa, Victoria Nuland siku ya Jumanne aliishutumu Urusi kwa kutaka kunufaika zaidi kutokana na ushiriki wake katika juhudi za kurejesha makubaliano ya nyuklia. Wapatanishi wa Ulaya kutoka Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani walijiondoa kwa muda katika mazungumzo hayo wakiamini wamefikia hatua nzuri na sasa ilikuwa jukumu la Marekani na Iran kukubaliana juu ya masuala ambayo hayajakamilika. Rais wa Iran Ebrahim Raisi kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema Iran haitolegeza msimamo wake katika mazungumzo hayo ya Vienna.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii