Nchi za Mashariki ya Kati zatafuta suluhu ya vita vya Iran

Waziri mkuu wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, amefanya mazungumzo mjini Tehran nchini Iran, katika juhudi za kupunguza mvutano kati ya Marekani na Iran.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Al Thani alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran, Abbas Araghchi, ambapo walijadili njia za kupunguza hali ya mivutano pamoja na pendekezo la Iran na Oman la kuhakikisha usalama wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

Ofisi ya Al Thani imesema kiongozi huyo alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya nchi jirani na kulinda uhuru wa usafiri wa meli katika eneo hilo.

Wakati wa ziara hiyo, Al Thani pia alikutana na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, pamoja na Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Qalibaf.

Mazungumzo hayo yanafanyika wakati Qatar ikiendelea kujitokeza kama mpatanishi katika juhudi za kupunguza mvutano na kuimarisha usalama wa usafiri wa majini katika eneo la Ghuba.


 

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii