Tshisekedi azindua mazungumzo ya kitaifa bila M23

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, amezindua rasmi mchakato wa mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya amani, mshikamano na ujenzi wa taifa.

Akilihutubia taifa kupitia televisheni ya umma, Tshisekedi amesema mazungumzo hayo yataanza katika majimbo yote 26 ya DRC kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kitaifa mjini Kinshasa, na kwamba mchakato huo utawakutanisha wawakilishi wa serikali, upinzani, mashirika ya kiraia, viongozi wa dini pamoja na makundi mbalimbali ya wananchi kwa lengo la kujadili mustakabali wa taifa.

Hata hivyo Tshisekedi, amesema kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda halitashiriki katika mazungumzo hayo ya kitaifa yanayolenga kuleta maridhiano nchini Kongo, akisema kuwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mjini Washington mwezi Desemba mwaka jana ndiyo mchakato unaofaa kushughulikia suala la M23.

Baadhi ya wanasiasa wa upinzani walipendekeza M23 na rais wa zamani Joseph Kabila washirikishwe katika mazungumzo hayo, lakini Tshisekedi amesisitiza kuwa nafasi ya kurejea katika jamii itaendelea kuwa wazi kwa wale watakaoachana na matumizi ya nguvu na kulaani vitendo vya uhasama.

Pata Habari Kupitia Mitandao Yetu Ya Kijamii