Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya Libya Stephanie Williams anajaribu kutafuta makubaliano mwezi huu kuhusu sheria za uchaguzi na mipango ya kikatiba nchini Libya, huku pande zinazozana zikiwa katika mzozo mkubwa. Akizungumza na shirika la habatri la Reuters Williams amesema anataka mazungumzo kati ya Wabunge na Baraza Kuu la Serikali, kufanyika kabla ya mwezi wa Kiisalam wa Ramadhan ambao unatarajiwa kuanza Aprili 1. Libya inakabiliwa na mzozo wa kisiasa baada ya bunge kuiapisha serikali mpya, huku utawala ulioko madarakani ukikataa kuachia madaraka kukiwa na msukosuko wa jaribio lililoshindikana la kufanya uchaguzi wa kitaifa mwezi Desemba.Alipoulizwa ni serikali ipi ambayo Umoja wa Mataifa unaitambua, Williams alisema umoja huo hauko katika biashara ya kuidhinisha au kutambua serikali bali unalenga kushinikiza uchaguzi.